Alipofika umri wa miaka 13, mama yake mpenzi alimpeleka
mjini kuendelea na masomo. Yeye hakuwa mgeni hapo mjini, kwani
Mwera ipo masafa ya maili 7 tu kutoka mji mkuu wa Unguja. Kwa vile
alivyokuwa akija mjini baadhi ya nyakati, aliweza kujuana na watoto
wengi wa makamo yake na kuchanganyika nao katika michezo.
Wakati huo, zilikuwa zikipitia Unguja meli za namna kwa namna,
kwani hii ilikuwa ikihesabika kuwa ni moja katika bandari mashuhuri
ya Afrika ya Mashariki. Pia zikiteremsha bidhaa za kila aina na
kuchukua zile za pande hizi. Nyingi katika meli hizo mpaka hivi leo zi-
natia nanga bandari hii ya Unguja. Kwa hivyo, hapo pwani zilizuka
kazi nyingi na vijana chungu nzima waliweza kujipatia kazi ya ku-
faa. Abeid naye pia alijitia humo pamoja na wananchi wenziwe. Kwa
vile alivyopata fursa ya kuzipandia meli nyingi, kukutana na
kuzungumza na wasafiri, mabaharia na wafanya kazi wa humo, ilimjia
hapo na yeye hamu kubwa ya kutaka kusafiri, kuona nchi za nje na
kuweza kushuhudia kwa macho yake namna mataifa mbali mbali
yanavyoishi katika dunia yetu hii.
Mawazo hayo yalimkaa sana moyoni mwake. Hapo alimkabili
mama yake mpenzi na kumweleza fikra na maazimio yake na alimtaka
ampe ruhusa kwa kuingia katika kazi za bahari. Bibi Amina al-
imkubalia mwanawe kuwa mwana wa bahari kwa kusikia kuwa safari
zake zitakuwa za zile nchi za jirani na ataweza kumwona mwanawe
kila mara meli yake itakapofika Unguja.
Katika 1920, Sheikh Abeid alitimia miaka 15 na hapo alipokelewa
na kampuni kufanya kazi katika merikebu zao zile zinazosafiria pwa-
nipwani ya Afrika ya Mashariki kwa kuipitia bandari kama zile za Dar
es Salaam, Mikindani, Mafia, Tanga, Mombasa na kadhalika. Sheikh
Abeid hufurahi sana meli yake inapofika Unguja, kwani hupata fursa ya
kumzuru mama yake mpenzi, wazee wengine na kuonana pia na
marafiki zake.
Baada ya miaka miwili, Sheikh Abeid katika 1922 aliingia ku-
fanya kazi katika meli za nje na zile zilizosafiria nchi za mbali. Humu
ndimo alimopata maarifa mengi na kuziona mwenyewe zile faida
nyingi za safari. Katika miaka 17 aliyoipitisha humo merikebuni kwa
kufanya kazi za namna mbali mbali, aliweza kuzitembelea nchi nyingi.