Wabantu kwa jumla ni wakulima wa nafaka kama vile mtama,
mawele na mahindi. Sehemu ambazo mbungo si kizuizi ng’ombe
wanafugwa. Pia mifugo ya kawaida ni mbuzi, kondoo na kuku. Mbwa
wengi wanaonekana bali paka ni adimu. Makabila yaliyo mengi huen-
desha uwindaji na utegaji wa wanyama na uvuvi huendeshwa katika
maziwa na mito na pwani ya Bahari ya Hindi.
Kwa kawaida makabila yote hupenda uimbaji wakijitengenezea
vyombo vyao. Chombo cha kawaida katika Afrika ya Kati na ya Kusini
ni aina ya marimba. Chombo hiki ni chombo cha ufundi wa asili wa Ki-
afrika, kwa vile hakipatikani mahali pengine po pote. Muziki unafanya
kazi katika maisha ya kila siku ya Mwafrika zaidi pengine kuliko watu
wengi duniani. Katika matukio ya maana yanayomtokea mtu, kama vile
kuzaliwa kwa mtoto, kuoa na mwishowe kifo, yote haya hushere-
hekewa kwa muziki na ngoma.
Makabila yote ya Tanzania hujenga nyumba, ingawaje baadhi ya
nyumba hizo ni ndogo. Makundi mengine hujenga vibanda vya muda
pamoja na nyumba za kudumu. Vibanda vya muda, ni kwa ajili ya
kulinda mazao yasiharibiwe na wanyama na kwa kupumzikia wakati
wa jua kali la mchana. Ingawaje mara nyingi nyumba ni hafifu katika
mjengo lakini zinafaa katika hali ya nchi ambayo si baridi. Pia lazima
tukumbuke kwamba katika maisha ya Kiafrika, muda utumikao kwa
kukaa ndani ni mdogo. Nyumba ni mahali pa kulala, kupikia na kulia
chakula nyakati za mvua. Ni mahali pa kuzalia, kuugulia na mwishowe
kufia. Kazi kubwa za maisha zinazohusiana na kutayarisha na kuyaan-
galia mashamba, kuwaangalia wanyama na kukusanya matunda na miti
mingine iliwayo, na mara kwa mara uwindaji na uvuvi, hizi zote
huchukua muda wote wa mchana. Kuamka mapema ni jambo muhimu
na majira ya giza ni kwa ajili ya kulala na kupumzika, ingawaje siku fu-
lani fulani ngoma na uimbaji huendelea usiku mzima. Ingawa kwa wa-
geni nyumba zaonekana zenye giza, kwa wakaaji wenyewe hazina to-
fauti, wao huridhika na mwangaza mdogo wa moto wa kupikia.
Kuna njia nyingi za ujenzi. Mara nyingi njia hizo hufuatana na
madhehebu ya kale, pamoja na aina za vifaa vipatikanavyo.
Katika Kijiji hiki cha Makumbusho baadhi ya aina hizi za nyumba
zimejengwa pamoja na sehemu ndogo ndogo za majengo hayo. Kuna
majengo ya ya makabila kama Wazaramu, Warundi, Wachaga,
Wanyakusa, Wanyamwezi, Wagogo na wengine.